MAJESHI YA UGANDA YALIVYOINGIA KAGERA
MWAKA 1978, Majeshi dhalimu ya Nduli Idi Amin Dadaa wa Uganga, yalivamia
Ardhi ya Tanzania, eneo la Mto Kagera, katika mkoa wa Ziwa Magharibi na
kufanya uharibifu mkubwa wa mali na kuua wananchi wa mkoa huo,
NYAKASAGANI MASENZA anasimulia kupitia vyanzo mbali mbali vya habari
jinsi majeshi hayo yalivyoingia Tanzania na Amin kutangaza rasmi kuwa
eneo hilo la Mto Kagera ni sehemu ya Uganda.
DAIMA Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwa ukombozi wa Bara la Afrika,
ikiwa miongoni mwa mataifa masikini zaidi duniani, lakini iliyojariwa
viongozi wenye hekima, kuanzia muasisi wake Hayati Mwalimu Julius
Nyerere, Rais wa pili Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya
Kikwete.
Busara za viongozi wa Tanzania zilianza kuonekana mwaka 1961, baada ya
Mwalimu Nyerere kuwanasua watanzania kutoka mikononi mwa utawala
kandamizi wa wakoloni, wakati huo pia akiwa tayari kuchelewesha Uhuru wa
Tanganyika ili nchi zingine zilizokuwa kwenye mchakato wa uhuru zipate
Uhuru siku moja na Tanganyika.
Msimamo dhabiti Mwalimu Nyerere, uliweza kujenga Tanzania imara na
kuifanya kuwa Taifa kimbilio la vikundi na vyama vya wapigania uhuru
Kusini mwa Afrika, ambao walipewa hifadhi ya kudumu na kutumia ardhi ya
Tanzania kuwa sehemu ya mapambano ya kudai uhuru wao, ambao waliupata
kupitia mgongo wa Tanzania.
Viongozi kama Hayati Edward Mondolane, Samora Macheli wa Msumbiji,
Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Yoweri Mseveni wa Uganda, ni sehemu ya
viongozi waliopitia mikononi mwa Mwalimu Nyerere wakati wakipigana nchi
zao zikombolewe.
Watanzania walianza kuingiwa na wasiwasi mwaka 1971, wakati Nduli Idi
Amin Dada alivyoasi na kuchukuwa madaraka ya Uganda kwa nguvu baada
kuungusha utawala halali wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hayati Milton
Obote na kutangaza kuitawala nchi hiyo kijeshi.
Mwanzo wa utawala wake waganda pamoja na mataifa mengine walidanganyika,
wakawa na matumaini makubwa juu ya kiongozi huyo wa kijeshi, kutokana
na ahadi zake nyingi kwamba yeye ataitala uganda na kuhakikisha eneo
lililoko Tanzania, sehemu ya mto kagera, katika mkoa wa Ziwa Magharibi
litakuwa sehemu ya Uganda.
Mwaka huo huo, Idi Amin alijaribu kutimiza madai yake kwa kuishambulia
sehemu hiyo ya Mto Kagera, lakini watanzania walikuwa imara katika
kulinda ardhi yao sehemu hiyo akashindwa, baada ya majeshi yake
kurudishwa nyuma na majeshi hodari ya Tanzania.
Pamoja na majeshi yake kurudishwa nyuma, Fashiti huyo aliyejitangaza
kuwa Rais wa maisha wa Uganda, akiwapongeza wapiganaji wake kwa
kurudishwa nyuma huku akiwasifia kupata jeraha kidogo kutoka kwa majeshi
ya Tanzania.
Baada ya wapiganaji wake kurudishwa nyuma Idi Amin alisema huo ni mwanzo
tu, awamu nyingine atatumia silaha nzito zaidi ikiwa pamoja na
makombola ya kurushwa kwa ndege na kuwaongezea nguvu askari wa miguu,
jambo ambalo liliwafanya waganda kuingiwa na hofu kutokana na utawala
huo wa mabavu, baada ya Amin kuanza kuwatilia shaka wananchi na kuwaua
hovyo.
Mauaji ya kinyama yakawa kitu cha kawaida katika Uganda, wananchi wengi
wasiokuwa na hatia walipoteza maisha, watu mashuhuri kama Jaji Mkuu
Benedicti Kiwanuka na Askofu Mkuu Jamal Luwumu, waliteswa na kuuawa
chini ya utawala wake.
Aitoa amri kuwa watu wote wanaopinga utawala wake, wapigwe risasi
hadhalani, katika kutekeleza moja ya ndoto zake alizodai kuwa ni
mazungumzo baina yake na Mwenyezi Mungu, aliwafukuza kutoka Uganda,
Waasia wote waliokuwa na pasi za kusafiria za Uingereza na kuwanyanganya
mali zao zote.
Baada ya shutuma nyingi za uongo dhidi ya Tanzania, mnamo tarehe 30
)ktoba 1978 Idi Amin aliyaamuru majeshi yake kuvuka mpaka na kulivamia
eneo la Tanzania, ambapo watanzania zaidi ya 10,000 wasiokuwa na hatia
yaliangamizwa na eneo la kilomita za mraba 1850 zilichukuliwa na majeshi
ya Uganda.
Majeshi hayo ya Amin yalilikalia eneo la mto Kagera sehemu ya kyaka na
kufanya vitendo vya kinyama kwa kuua wananchi wa mkoa wa Ziwa Magharibi
hovyo, kuchoma nyumba, viwanda, kupora mali nyingi na kuzipeleka Uganda.
INAENDELEA
1 Maoni yako: